Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema haijazuia biashara ya mazao ya Misitu huku ikiwataka wafanyabiashara wa mazao ya misitu kufuata Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuweka usawa katika biashara pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Costantino Mwakamo, aliyetaka kujua kauli ya Serikali juu ya Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania – TFS.
Amesema, “Sheria ya Misitu Sura ya 323 na Kanuni zake za mwaka 2004 zimeelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuvuna, kusafirisha na kuuza mazao ya misitu kwa kuzingatia umiliki wa misitu/miti ambao ni ya watu binafsi, Serikali za vijiji, Serikali za mitaa au Serikali Kuu.”
Kuhusu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Agnes Marwa juu ya Serikali kuwatafutia eneo mbadala Wananchi wa Vijiji vya Kata ya Nyantwari Bunda, wanaofanyiwa uthamini kupitisha uhifadhi, Masanja amesema zoezi hilo lipo katika hatua za mwisho na baada ya hapo Wananchi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria.