Shirika la Uzalishaji Mali la Suma JKT limetangaza orodha ya majina ya wadaiwa wake sugu wa matreka ambapo wako mawaziri wa sasa, mawaziri wastaafu, wabunge na wakuu wa mikoa.
Orodha hiyo imetolewa kufuatia agizo la Rais John Pombe Magufuli wakati wa uzinduzi wa kituo cha Uwekezaji cha Suma JKT ambapo Mkuu wa Majeshi alimuomba Rais asaidie kuhakikisha wadaiwa wote wanalipa madeni yao.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo amesema Suma JKT wanazidai taasisi binafsi Sh.bilioni 40 na taasisi za umma sh.bilioni 3.4.
Baadhi ya majina ya mawaziri wa sasa yaliopo kwenye orodha hiyo ni Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Luhaga Mpina na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Kangi Lugola.
Pia kwenye orodha hiyo yumo Naibu Waziri wa Wizara ya Uvuvi na Mifugo Abdallah Ulega ambaye ni Mbunge wa Mkuranga.
Mawaziri wastaafu waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Dk.Juma Ngasongwa ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda Biashara na Waziri wa Wizara mbalimbali kwenye Serikali zilizopita.
-
Video: Kauli za wabunge mwiba kwa Dk. Mpango, Mawaziri nao ndani wadaiwa sugu JWTZ
-
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 27, 2018
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato mkoani Geita naye ametajwa kwenye orodha hiyo.
Mbali na viongozi hao Suma JKT inazidai Taasisi 26 zikiwemo Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali, Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Wizara ya Afya Maendeleo ya jamii, jinsia , wazee na watoto, Chuo Kikuu Huria (OUT), Taasisi ya Elimu, Chuo cha Taifa cha Utalii, Mamlaka ya Rufaa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Wizara ya Ardhi.
Mwingine alkiyetajwa kwenye orodha hiyo yenye jumla ya majina 1392 ni aliyekuwa waziri wa fedha kwenye utawala wa awamu ya nne, Mustapha Mkulo.
Wakuu wa Mikoa wa sasa waliotajwa kweney orodha hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka na Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Rehema Nchimbi.
Wabunge waliotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Husna Mwalima wa Kigoma Kusini (CCM), Mbunge wa Shinyanga Mjini Steven Maselle (CCM) na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM).