Mwimbaji wa kike aliyeshirikishwa na Diamond Platinumz kwenye ngoma kubwa ya ‘Nitarejea’, amegeuka kuwa muathirika mkubwa wa pombe haramu aina ya gongo huku akiomba msaada aweze kuachana na ulevi wa kupindukia.
Hawa ambaye sauti yake iliwateka wengi na kumtabiria makubwa kwenye muziki wakati audio na video ya ‘Nitarejea’ inaachiwa mwaka 2014, ameonekana kupitia kipindi cha ‘Shilawadu’ cha Clouds TV akiwa amedhoofu mwili huku mama yake mzazi akieleza kuwa hata akili yake haiko sawa kutokana na kuathiriwa na unywaji wa pombe hiyo haramu.
Msanii huyo ambaye aliweka wazi kuwa mbali na kushirikishwa na Diamond kwenye wimbo huo alikuwa mpenzi wake, alieleza chanzo cha kujitumbukiza kwenye unywaji wa gongo akidai kuwa ilitokana na kuzoea kunywa pombe kali za gharama kubwa na kuzizoea lakini baadae hakuweza kumudu gharama yake baada ya mpenzi wake aliyekuwa akimnunulia kuachana naye na yeye kukumbwa na ukata.
Alieleza kuwa alianza kunywa vinywaji vikali vya gharama kubwa alipokuwa karibu na familia ya mzee Zahir Zorro kwa lengo la kujifunza muziki. Alisema baadae alimpata mpenzi wake aliyekuwa rafiki wa Maunda Zorro, mwanaume ambaye alimnunulia vinywaji hivyo kwa wingi.
“Baada ya kuachana naye na tayari alikuwa ameshanipa mimba nikamzalia mtoto, sasa mpunga [fedha] wa kununua zile pombe kali nikawa sina, na ile addiction sasa ndio nikajikuta nimeanza kunywa gongo kutafuta ile stimu,” alisema.
Aidha, Hawa alifafanua kuwa ingawa alishaolewa na kuachika, hana tatizo lolote na Diamond na kwamba hata wakati wa mchakato wa harusi yake iliyofanyika mwaka 2015 alimtafuta mkali huyo wa ‘Eneka’ ili amuombe mchango wa harusi lakini hakuweza kumpata.
Alisema kutokana na hali ngumu inayomkabili kuna wakati anatamani angekuwa bado mpenzi wa Diamond na kumzalia mtoto kama mama Tiffah [Zari], lakini tayari sio riziki yake.
Rama Dee awaomba msamaha mashabiki, Clouds FM kuhusu ‘Anti-Virus’
Aidha, mama yake mzazi alieleza kuwa hata alipojifungua mtoto wake, mama mzazi wa Diamond alifika nyumbani kwao mara mbili akiwasilisha zawadi ya nguo akidhani mtoto huyo ni mwanae, lakini Hawa alisisitiza kuwa mtoto huyo sio damu ya Chibu.
“Mama yake Diamond alikuja hapa mara mbili akileta nguo akidhani ni mtoto wa Diamond lakini huyu alikataa. Kwahiyo, mama Diamond hakuwahi kuja tena hapa tangu wakati huo,” mama Hawa alisema.
Hata hivyo, msanii huyo wa kike alisisitiza kuwa yuko tayari kuachana na matumizi ya gongo na kuyaanza maisha mapya ya muziki na ya kijamii, huku akiomba wasamalia wema waweze kumsaidia kumpeleka katika nyumba maalum ya kutibu hali hiyo, maarufu kwa lugha ya kigeni ‘Sober House’.
‘Shilawadu’ walifanikisha kumpata mmoja kati ya wamiliki wa sober house aliyeweka wazi kuwa atajitolea kumtibu Hawa kwani ndicho kitu hasa wanachokifanya kuwarusha waliopotezwa na matumizi ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia katika maisha ya kawaida.