Uongozi wa Klabu ya Singida Fountain Gate umeweka wazi mipango na matarajio yao kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Singida Fountain Gate inayonolewa na Kocha kutoka nchini Uholanzi Hans van Der Pluijm imekusudia kufanya makubwa zaidi ya msimu uliopita, ambapo ilimaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu, ikitanguliwa na Azam FC, Simba SC na Mabingwa Young Africans.
Afisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Masanza amesema, amesema kikosi chao kipo katika hali nzuri na kimejipanga kupambana ili kuvuka malengo ya msimu uliopita.
Amesema dhamira yao ni kumaliza nafasi tatu za juu kama sio kutawazwa kuwa Mabingwa wa Tanzania Bara msimu ujao, ambao umepangwa kuanza Agosti 15.
“Timu yetu inajiandaa vyema na msimu ujao tukiwa na mikakati mizuri. Hakuna majeruhi kwa sasa wachezaji wanaendelea vizuri na mazoezi tunaomba mashabiki watuunge mkono katika mashindano ninaimani tutafanya vizuri katika mashindano ya ligi.
“Mpago mkubwa ni kufanya vizuri kwenye mashindano ambayo tunashiriki. Wachezaji wapo tayari na tunaamini itakuwa hivyo licha ya ushindani kuwa mgumu tupo tayari.” Amesema Masanza
Kikosi cha Singida Fountain Gate kwa sasa kipo jijini Tanga, tayari kwa mchezo wa Nusu Fainali, Ngao ya Jamii ikianza dhidi ya Simba SC, utakaopigwa Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga Alhamis (Agosti 10).