Uongozi wa Tanzania Prisons umesema umeandaa vyema kikosi chao na unaahidi kufanya mapinduzi makubwa katika msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 15, mwaka huu.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Ramadhani Nyamka, amesema malengo ya timu yao ni kushika nafasi ya juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Nyamka amesema wamejiandaa kuonyesha soka la ushindani na malengo yao ni kupata tiketi ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa hapo mwakani.
“Tumejipanga kufanya mapinduzi makubwa, mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani, tunaimani na benchi letu la ufundi,” amesema Nyamka.
Ameongeza wamefanya usajili mzuri ambao utawasaidia kupata ushindi katika kila mechi na hawana mpango wa kusajili wachezaji wa kigeni kwa sababu malengo yao ni kusaidia kuinua na kuendeleza vipaji vya nyota wa Kitanzania.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Wakazi Supply, Kelvin Ndawi, ambao ndio wamewatengenezea jezi amesema wataendelea kufanya kazi na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.
“Hizi jezi zina ubora wa hali ya juu, naamini kila shabiki atazipenda, wataingia nazo uwanjani kama sehemu ya kuwapa Hamasa wachezaji,” Ndawi amesema.