Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, amemuagiza Mtendaji Mkuu mpya wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila, kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali zinazozikabili wakala huo, ili kuendeleza heshima iliyojijengea kwa wadau wake hapa nchini na kimataifa.

Waziri Chamuriho ametoa agizo hilo huyo jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kumkabidhi ofisi Mtendaji Mkuu huyo, ambapo pamoja na mambo mengine amemtaka kuhakikisha kuwa anasimamia vema mtandao wa barabara nchini wenye jumla ya urefu wa kilometa 36,000.

“TANROADS inasimamia ujenzi wa barabara hizi kwa kiwango cha lami, ujenzi wa madaraja na matengenezo ya barabara, hivyo hakikisheni zinapitika muda wote, pamoja na kuhakikisha magari yanayopita katika barabara hizi hayazidishi uzito kwa kusimamia vyema mizani zote nchini,” Amesema Waziri Chamuriho.

Mbali na hilo, Waziri Chamuriho, amewasisitiza pia kuhakikisha wanapunguza malalamiko mbalimbali ikiwamo ucheleweshaji wa miradi inayosababishwa na kuchelewa kwa misamaha ya kodi, ujenzi wa barabara chini ya kiwango na ucheleweshaji wa malipo ya fidia  kwa wananchi wenye haki ya kulipwa ambao wanapisha miradi mbalimbali ya  ujenzi inayosimamiwa na Wakala huo.
 
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila. amemuhakikishia Waziri Chamuriho kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kutoa ushirikiano kwa  watumishi waliopo chini yake, kwani amekuwa katika sekta hiyo kwa muda mrefu, hivyo anazifahamu changamoto zote zilizopo.

Rais Samia aongoza viongozi kuaga mwili wa marehemu Kwandikwa
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 6, 2021