Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha wanasimamia na kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika mikoa yao kwa kuwa kazi ya kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta ni kushughulikia migogoro ya vijiji 975.
Ameyasema hayo leo Oktiba 11 wakati akifanya mazungumzo na viongozi, wabunge pamoja na watendaji wengine katika Mkoa wa Tabora wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta mkoani hapo.
” Kamati yetu ya Mawaziri nane itaendelea kwa vile vijiji 975 ila kazi ya kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi itaendelea kwa usimamizi wa wakuu wa mikoa na kama ipo sababu ya msingi ya kuondoa baadhi ya vijiji basi mkoa utainisha kwa kuwa kilichofanyika sasa hivi ni huruma ya Rais,” Amesema Waziri Lukuvi.
Amesema kila mkoa Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanapopita wanaacha timu ya wataalamu ili kuangalia namna bora ya utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya ardhi katika vijiji kwa maslahi mapana ya Taifa.
Katika kuelezea zaidi Waziri Lukuvi amesema kilichofanyika kumega sehemu maeneo ya hifadhi ni huruma ya Rais na kusisitiza kuwa, kama eneo ni chanzo cha maji basi eneo hilo linahitaji kutunzwa na kusisitiza kuwa ni aibu kuendelea kuwepo migogoro ya ardhi ikiwemo ile ya mipaka katika mikoa na kutaka migogoro ya ardhi kumalizwa kwa mfumo huo.
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja aligiza taasisi zilizoko chini ya wizara yake kuacha kuwasumbua wananchi wanaoishi maeneo ya hifadhi kipindi hiki ambacho kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanazunguka katika mikoa mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo.