Wabunge wa Chadema ambao walitakiwa na Mahakama kukamatwa kwa kukiuka masharti ya dhamana wameendelea kujisalimisha baada ya Halima Mdee jumamosi, leo Mbunge John Heche wa Tarime vijijini na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa mjini wamejisalimisha na kukamatwa na polisi baada ya kufika.
Novemba 15 mwaka huu Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ilitoa amri ya wabunge wanne wa Chadema kukamatwa kwa kuvunja masharti ya dhamana kwani hawakuwepo siki hiyo Mahakamani hapo na hata wadhamini wao pia hawakuwepo.
Mdee ameunganishwa pia na wabunge hao wawili waliojisalimisha leo kufikishwa Mahakamani mapema asubuhi akitokea kituo cha Polisi Oysterbay.
Imeelezwa kuwa washtakiwa hao watafikishwa Mhakamani kesho Novemba 19, 2019 katika kesi ya uchochezi inayowakabili.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, naibu katibu mkuu, Salum Mwalimu, Katibu mkuu wa chama hicho, Vicent Mashinji, Easter Matiko, Easter Bulaya na John Myika.
Wote wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kusababisha hisia za chuki pia makosa ya uchochezi yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es salaam.