Kufuatia kifo cha Suguta Chacha mdogo wa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliyeuawa kwa kuchomwa kisu cha mgongoni huku akiwa amefungwa pingu, familia imekubali kuuzika mwili huo na mapema leo hii wamekataa kupokea msaada wa chakula kutoka ofisi ya Kamanda wa polisi wa kanda ya kipolisi ya Tarime Rorya.
Imekuwa taratibu kwa Serikali kutoa msaada wa hali na mali pale inapokuwa imehusika moja kwa moja na tukio fulani, au raia wake kukutwa na majanga fulani, kama Serikali huchukua jukumu la kuonesha mchango wao kuonesha wapo pamoja na familia iliyokumbwa na majanga.
Utaratibu huo umekuwa tofauti kwa familia ya Chacha waliompoteza ndugu yao mikononi mwa Polisi, Suguta Chacha, hivyo familia imetoa msimamo wake na kudai kuwa ipo tayari kupokea msaada kutoka kwa mtu yeyote lakini siyo jeshi la polisi.
Msimamo huo umetolewa na katibu wa Ukoo, Chacha Heche, Aidha mazishi ya ndugu yao yanatarajia kufanyika Alhamisi ya wiki hii katika kijiji cha Nyabitocho.
Mtuhumiwa wa mauaji hayo tayari ametiwa hatiani na ameshitakiwa kwa kesi ya mauaji.