Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri Hector Cuper, amesema huenda mshambuliaji Mohamed Salah akacheza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi, wakati wa fainali za kombe la dunia, lakini akawahusia wachezaji wengine kutoweka matumaini makubwa ya kumtegemea mshambuliaji huyo wa klabu ya Liverpool.
Salah bado anaendelea kuuguza majeraha ya bega lake la kushoto baada ya kufanyiwa matibabu juma lililopita nchini Hispania, na tayari ameshatangazwa kuwa sehemu ya kikosi cha mwisho cha Misri kitakachoshiriki fainali za kombe la dunia.
“Ni matarajio yetu kumuona anacheza mchezo wa kwanza hatua ya makundi, lakini hatutaki kumuharakisha, endapo atakua tayari kucheza atacheza,” kituo cha televisheni cha Sky Sports kimemnukuu Cuper.
“Ni mchezaji muhimu sana katika kikosi cha Misri, lakini kuna haja kwa wachezaji wengine kutambua nao wana umuhimu mkubwa, na watapaswa kucheza bila Salah, endapo hatokua FIT kwa mchezo wa kwanza.
“Huu ni mchezo wa soka, una matukio mbali mbali likiwepo hilo la kuumia kama lililomkuta Salah, hivyo kila mmoja anapaswa kulibeba na kutambua umuhimu wake kikosini, huku tukimuombea mwenzetu apone kwa haraka.”
Katika hatua nyingine kocha huyo kutoka nchini Argentina, akazungumzia maendeleo ya Mohamed Salah kwa kusema “Salah yupo katika hatua nzuri za kupona jeraha lake baada ya kupatiwa matibabu siku kadhaa zilizopita,”
“Bado ninasisitiza kama atakua tayari kucheza mchezo wetu wa kwanza wa hatua ya makundi atacheza, lakini kama hatokua tayari ataendelea kusubiri.”
Timu ya taifa ya Misri imepangwa kundi A katika fainali za kombela dunia 2018, inatarajia kucheza mchezo wa kwanza katika kundi hilo Juni 15, dhidi ya timu ya taifa ya Uruguay mjini Ekaterinburg.