Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Hemed Morocco amesema hali ya kukosa ushindi mfululizo katika timu hiyo inatokana na kikosi chake kukosa wachezaji wenye ubora wa kupambana katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Morocco ameyasema hayo baada ya timu hiyo kukosa ushindi katika mechi zake nane mfululizo kati ya tisa ilizocheza mpaka sasa, hali iliyosababisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita, Zahara Michuzi kumtaka kocha huyo kuonana naye kujieleza.
Morocco amesema hajawahi kuwa na matokeo mabovu kiasi hicho, lakini ubora mdogo wa wachezaji unachangia matokeo hayo na sasa akijipanga kuongeza idadi ya wachezaji wanne mpaka watano wakati wa usajili wa dirisha dogo ili kuhakikisha wanakuwa bora mzunguko wa pili.
Amesema katika mechi za kwanza wachezaji hao walionesha ubora mkubwa, lakini wamekuwa wakishuka viwango siku zinavyosonga na zaidi makosa ya mchezaji mmoja mmoja ndio yamekuwa yakiwagharimu.
Kocha huyo alipoulizwa kama alishakutana na Mkurugenzi Michuzi, amesema hayuko tayari kulizungumzia hilo kwani ameamua kukaa kimya.
Geita ambayo imeshinda mechi moja, sare nne na kufungwa mara nne, inashika nafasi ya 15 kati ya timu 16 ikiwa na pointi saba.