Kocha Msaidizi wa Taifa Stars Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema wamekuwa wakiifuatilia Niger kwa ajili ya kujua mbinu zao na aina yao ya Uchezaji ili wajue wanawakabili vipi Jumamosi (Novemba 18) ugenini katika mechi ya kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Tayari Taifa Stars ipo kambini jjini Dar es salaam ikiendelea na mazoezi katika Uwanja wa JKT uliopo Kunduchi, kujiandaa na mchezo huo wa ugenini na kurejea nyumbani kuikaribisha Morocco katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha huyo amesema karibuni wachezaji wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wamewasili, na mazoezi makali yanaendelea kuwaweka sawa wachezaji, huku tayari wakiwa wameshatuma watu kwa ajili ya kuendelea kuisoma Niger.
“Mazoezi yanaendelea vizuri, ushindani ni mkubwa na ni kitu kizuri kwetu sisi, kila mchezaji anaonekana anataka kupata nafasi, nao pia wanajua umuhimu wa hizi mechi.
“Tumekuwa na mazoezi mara mbili kwa siku, asubuhi wachezaji wanakwenda Gym, jioni tunakwenda Uwanjani, unajua kwa bahati nzuri tunacheza na timu ambayo tulikuwa nao kundi moja kwenye kufuzu AFCON kwa hiyo kwanza tunawajua vizuri, na bila shaka tunawafuatilia ambavyo inawezekana ili kujua walivyo, na sisi kuingia vipi kuwakabili,” ametamba Morocco.
Kwa upande wa Mshambullaji wa Taifa Stars, Simon Msuva amesema mechi yao dhidi ya Niger haitakuwa rahisi kwa sababu timu hizo zinajuana na aliwahi kuwafunga bao 1-0.
Amesema wamekuja kufanya kazi kupambania taifa katika michezo hiyo miwili wakianza na Niger utakaochezwa Jumamosi (Novemba 18) kabla ya kuikaribisha Morocco Jumanne (Novemba 21) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.