Kocha Mkuu wa Namungo FC Hemed Morocco amesema kikosi chake kipo katika hali nzuri kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa sita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utawakutanisha dhidi ya Young Africans Jumamosi (Novemba 20) Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Kocha Morocco amesema amekitumia kipindi cha mapumziko ya Ligi Kuu kukiandaa vizuri kikosi chake, na anaamini mapungufu aliyoyafanyia kazi yataleta matokeo chanya kwenye mchezo huo.

Hata hivyo Kocha huyo kutoka Visiwani Zanzibar amekiri Young Africans ina kikosi bora na imara, na hatua ya kuanza kwao vizuri Ligi Kuu msimu huu ndio imekua chagizo la kukiandaa vyema kikosi chake.

Lakini pamoja na kukiri huko, Morocco amesema ameona kuna mapungufu kadhaa kwenye kikosi cha Young Africans, na ametumia mwanya huo kutengeneza mbinu ambazo zitasaidia kupata alama tatu siku ya Jumamosi.

“Yanga imeanza vizuri na kuonekana bora, ukiangalia kiufundi hawajakamilika kwa asilimia zote, wanaupungufu ambao tutautumia kutafuta matokeo chanya ili kuondoka na alama tatu katika mchezo huo,” amesema Morocco.

Amesema wanaiheshimu Young Africans, lakini hawataiogopa na anatarajia mchezo huo utakuwa mzuri kwa sababu ya aina ya wachezaji walikuwa nao.

“Hatuwezi kuweka silaha zetu kwa wapinzani wetu, ila tunaingia kwa staili nyingine na mbinu tofauti na mechi tano tulizocheza. Tumejiimarisha kila idara na hatutowapa nafasi washambuliaji wa wapinzani kuleta madhara katika eneo letu ili kuhakikisha tunapata pointi tatu katika mchezo huo na kujiweka sehemu salama katika msimamo.” amesema Morocco.

Kabla ya kusimama kwa Ligi Kuu, Namungo FC walipoteza mchezo dhidi ya Mabingwa Watetezi Simba SC kwa kufungwa bao 1-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Young Africans wakiichapa Ruvu Shooting mabao 3-1.

Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 15, huku Namungo FC ikiwa nafasi 11 kwa kuwa na alama 5.

Hitimana: Ninajifunza mengi kwa kocha Pablo
Justine Bieber kuileta ziara yake Barani Afrika.