Baada ya kuambulia kisago cha bao 1-0 dhidi ya Mabingwa wa Watetezi Simba SC, Kocha Mkuu wa Namungo FC Hemed Morocco ametaja sababu zilizokikwamisha kikosi chake kwenye mchezo huo.

Namungo FC walikua wageni wa Simba SC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jana Jumanne (Novemba 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Morocco, amesema kilichowaponza kupoteza alama tatu mbele ya Simba SC ni ukosefu wa umakini kwa wachezaji wake dakika za mwisho, ambapo waliamini kazi imekwisha.

“Kupoteza umakini kwa wachezaji wangu kumefanya tukapoteza mbele ya Simba SC.”

“Tulianza kwa kasi kipindi cha kwanza na tukakubaliana kwamba inabidi tuzuie kwa kuwa Simba ilikuwa na hasira hasa baada ya kushindwa kupata matokeo kwenye mechi yao iliyopita.”

“Mpango kazi ulikubali kipindi cha kwanza tukarudi tena kipindi cha pili. Lakini sasa nguvu ilipungua baada ya mchezaji wetu mmoja kuonyeshwa kadi nyekundu.”

“Yote kwa yote naweza kusema kwamba nawapongeza Simba kwa kuwa wameshinda nasi tunajipanga kwa ajili ya mechi zijazo kwani ligi bado haijaisha na tupo kwenye mpango wa kuendelea kupata ushindi,” amesema Morocco

Bao la Simba SC kwenye mchezo huo, lilipatikana dakika ya 90, kupitia kwa Mshambuliaji wao kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere, baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Matola: Tutapata ufumbuzi wa tatizo letu
Kesi ya Mbowe na wenzake kuendele leo shahidi awasili Mahakamani