Imeelezwa kuwa Beki kutoka DR Congo Henock Inonga Baka, anatarajia kurejea dimbani mapema zaidi ya ilivyodhaniwa, kufuatia jeraha lake kuendelea vizuri.
Daktari wa klabu hiyo, Edwin Kagabo, amethibitisha kuwa beki huyo atarejea juma lijalo kwani maendeleo ya jeraha lake ni mazuri, akisema hakuumia sana kama watu wengi walivyodhani.
“Mpira wa miguu ni wa kugusana, nadhani baada ya wachezaji wenzake kufika pale na kuona damu nyingi iliyokuwa inatoka kwenye jeraha walionekana kushtuka sana na ndiyo iliwapa picha mashabiki jukwaani na waliokuwa wanatazama kwenye televisheni kuona kama ameumia sana au amevunjika.
“Kilikuwa kidonda chenye sentimeta 10 kwa nne, Urefu na upana, matibabu yake ni kwamba alishonwa nyuzi 13, lakini kila kitu kwenye matibabu kilikwenda vizuri,” amesema daktari huyo.
Amesema itamchukua Inonga juma moja na nusu kupona na kuanza mazoezi, lakini siku hizo zinahesabika tangu alipoumia.
Simba SC ilicheza dhidi ya Coastal Union Alhamisi iliyopita Uwanja wa Uhuru na kushinda mabao 3-0 na kwa mujibu wa daktari huyo siku hizo zinahesabika tangu alipoumia, hivyo ina maana juma lijalo ataanza mazoezi na wenzake.
“Kidonda chake kilikuwa kwenye mguu wake wa kulia hali yake kwa ufupi inaendelea vizuri, sasa hivi tunadili zaidi na kuuguza jereha lake na kwa hali ilivyo inaashiria uponaji wake utakuwa mzuri na wa haraka zaidi,”
“Kwa sasa tunahakikisha tunaweka dawa, kukifunga na kukifungua pamoja na matibabu mengine kama vile kumpa anywe dawa za kuua bakteria na za kutuliza maumivu, pengine Mungu akipenda ndani ya juma moja na nusu tangu alipoumia atakuwa tayari kurejea kwenye uwanja wa mazoezi,” amesema Kagabo.
Kuhusu majeruhi mwingine, Aubin Kramo, amesema bado anaendelea na mazoezi na siku si nyingi watawatangazia wanachama na mashabiki wa Simba ni lini na yeye atarejea uwanjani.
“Kramo alipata matatizo ya goti siku 20 zilizopita na yeye anaendelea na matibabu vizuri kabisa, kuna hatua tukifika ndiyo tutajua ni lini atarejea uwanjani ila kwa sasa bado tupo katika hatua ya mwanzo ya matibabu,” amebainisha daktari huyo.
Katika mechi yake ya kirafiki kabla ya kuivaa Power Dynamos ya Zambia, Oktoba Mosi Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam katika mechi ya mkondo ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC jana Jumanne (Septemba 26) asubuhi, iliirarua Pan African inayocheza Ligi ya Championship mabao 4-0.
Mabao ya Simba yaliwekwa nyavuni na Saido Ntibazonkiza, Moses Phiri, Kibu Denis na Willy Onana.
Wakati huo huo, timu ya Power Dynamos imeelezwa inaweza kumkosa kipa wake namba moja, Lawrence Mulenga, katika mechi ya marudiano dhidi ya Simba SC Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam.
Kipa huyo aliyeokoa hatari nyingi na kuinyima Simba SC ushindi wa ugenini aliumia katika mechi ya Ligi Kuu ya Zambia dhidi ya Zesco na kukimbizwa hospitalini, mchezo huo ukimalizika kwa sare ya mabao 2-2 kama ilivyokuwa katika matokeo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.