AMEBAKI staa mmoja tu kati ya watatu waliosajiliwa na Yanga kuthibitisha ubora wake, huku wawili kati ya hao wakitoa majibu kwamba jamaa wanastahili kuvaa uzi wa timu hiyo, lakini bosi aliyesimamia dili za usajili huo amefunguka hesabu zao zilivyokuwa na kuchimba mkwara mapema.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said amesema kila usajili katika mastaa watatu waliotua kwenye dirisha dogo akiwamo mshambuliaji Kennedy Musonda, kiungo mzawa Mudathir Yahya na beki Mamadou Doumbia ulikuwa na hesabu zake tofauti ndani ya timu hiyo mbali na kipa Metacha Boniface Mnata aliyenaswa dakika za mwishoni ili kuja kuziba pengo la Abdultwalib Mshery aliye majeruhi.
Hersi alisema awali kabla ya dirisha kufunguliwa hawakuwa na hesabu zozote za kusajili kiungo wa kati, ila walilazimika kufanya usajili huo wakimleta Mudathir kufuatia kuibuka sintofahamu ya kiungo wao Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambaye hadi sasa bado hajaripoti kambini tangu atangaze kuvunja mkataba na kuburuzwa mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).
“Fei ni mchezaji wetu hilo halina ubishi, lakini kutokana na sintofahamu aliyoiibua ilikuwa ni lazima kama klabu tufanye uamuzi wa kuangalia nani bora ambaye anaweza kuja nyakati hizi ili maisha yaendelee,” alisema Hersi ambaye hakuna staa wa Young Africans aliyetua klabuni hapo bila ushawishi wake.
“Tulipokaa na makocha walisema tukawaletee Mudathir, ingawa wasiwasi ukawa ni juu ya muda ambao alikuwa amekaa nje lakini baada ya kumsajili nafikiri kuna kundi kubwa la wachezaji wanaweza kujifunza kitu kwa kiungo huyu,” alisema Injinia Hersi.
“Mudathir baada ya kucheza mechi tatu tu amethibitisha kwamba yeye ni dhahabu, naamini na kwa makocha tulionao ambao wanajua kuwatoa wachezaji kutoka kiwango cha chini na kuwapandisha juu, muda si mrefu atakuwa bora zaidi ya hapa.”
Akifafanua usajili wa Musonda, Hersi amesema usajili wa Mshambuliaji huyo kutoka nchini Zambia ulikuja katika kumpunguzia mzigo Fiston Mayele ambaye kwa muda mrefu alikosekana mshambuliaji mwenye ubora kama wake ili kumpa ushindani.
“Makocha waliona kuna haja ya kuleta mtu kama Mayele ambaye hata siku akiumia kuwe na atakayechukua nafasi yake, lakini makocha walikuwa wanataka mshambuliaji wa namna hiyo katika kutanua mifumo yao zaidi, tukamuona Musonda,” alisema Hersi na kuongeza;
“Ila huyu Musonda ilikuwa ni vita kubwa kumpata, haikuwa kazi rahisi, tulilazimika kupambana hasa kupata huduma yake kwa kuwa tayari wapinzani wetu kwenye mashindano ya CAF klabu ya TP Mazembe walikuwa na hesabu naye.”
Akizungumzia ujio wa Doumbia, alisema beki huyo licha ya mapambano makubwa waliyoyafanya na Shirikisho la Soka la Mali, ujio wake ni maalum kwa mashindano ya CAF ambapo Yanga itashiriki hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho.
“Doumbia ni usajili tuliouhitaji kwa ajili ya mashindano ya CAF, tunajua aina ya wapinzani ambao tunakwenda kukutana nao, lakini makocha walihitaji mtu ambaye atakuja kuwa kitu kikubwa cha kuimarisha zaidi ukuta wetu,” alisema Hersi na kuongeza;
“Usajili huu haikuwa rahisi kutokana na kupishana kwa madirisha ya usajili kwa hapa kwetu na kule Mali anakotoka, nafikiri ni nafasi kwa shirikisho letu kuangalia namna ya kuweza kwenda sawa na mashirikisho mengine, wenzetu wa Mali waligoma kumuachia wakiomba huyu beki abaki kucheza mechi za CHAN lakini shida ikaja huku kwetu dirisha linafungwa.
“Nadhani hizi ni sajili ambazo zinakwenda kutuimarisha zaidi ya tulipokuwa, hao wachezaji waliokuja wakiunganika na watakaowakuta tunakwenda kuwa na timu ngumu ambayo itakwenda kupigana kwa kuthibitisha malengo yetu.”