Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM, Mhandisi Hersi Said amesema klabu ya Young Africans haijutii kumkosa kiungo mshambuliaji kutoka nchini Zambia Larry Bwalya alietua kwa watani zao wa jadi Simba SC mwanzoni mwa msimu huu.

Hersi ametoa kauli hiyo kufuatia kiwango cha kiungo huyo kuendelea kuwa kivutio kwa mashabiki wa soka la Bongo ambao wamekua wakimfuatilia kwa ukaribu Bwalya, na wengine kusema Young Africans walimkosa mtu muhimu kwenye kiosi chao.

Hersi amesema ni kweli walihitaji kumsajili Bwalya kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na walifikia hatua ya kuzungumza na mchezaji huyo akiwa kwao Zambia, lakini baadhi ya taratibu zilizohitajika kutoka kwenye klabu yake, ziliwakwamisha na kuamua kuachana naye.

“Larry Bwalya ni kweli tulifanya nae mazungumzo katika hatua ya mwanzo lakini ofa kutoka klabuni kwao ilikuwa kubwa sana na kwetu tuliiona kuwa haiendani na bajeti yetu ya usajili.

“Wakati tunamtaka sisi alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja ambao tulitakiwa kuuvunja kwa kulipia vipengele vitatu ambavyo vilikuwa kwenye mkataba wake ambavyo ni fedha ya uhamisho ambayo ingeenda kwa klabu yake, fedha ya kusaini mchezaji ambayo ingeingia moja kwa moja kwa mchezaji na fedha ya wakala jambo ambalo tuliona kama tungepigwa kwa kuwa ilikuwa ni fedha ndefu.”

“Hatujutii kumkosa Bwalya kwa kuwa si mchezaji wetu na bado tunaongoza ligi,”alisema Hersi.

Bwalya amekua msaada mkubwa kwenye kikosi cha Simba SC tangu alipojiunga na klabu hiyo mwezi Agosti mwaka 2020, na alitangazwa kuwa mchezaji bora wa michuano ya Simba Super Cup iliyomalizika mwishoni mwa juma lililopita jijini Dar es salaam.

Munir El Haddadi kucheza Morocco
Rage: Young Africans lipeni deni la Tambwe