Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Young Africans Hersi Ally Said amesema klabu hiyo haitafanya usajili ama kuwaacha baadhi ya wachezaji wanaomaliza mitakaba yao kwa kukurupuka, na badala yake itafuata mpango iliyojiwekea kuelekea msimu mpya wa 2022/23.
Baadhi ya wachezaji wa Young Africans wanamaliza mikataba yao, huku kukiwa hakuna harakati zozote hadi sasa zakusainishwa mikataba mipya, hali ambayo imezua taharuki kwa baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo.
Hersi amesema Young Africans imejipanga kuwa na kikosi imara msimu ujao, hivyo suala la kuwasainisha mikataba mipya wachezaji wanaomaliza mikataba yao ya awali litakuwa na utaratibu wake, ili kuzingatia mpango wa kuwa na kikosi imara.
Amesema kuna uwezekano mkubwa msimu ujao klabu yao ikarejea katika Michuano ya Kimataifa, hivyo dhamira yao ni kuwa na kikosi bora na imara kwa michuano ya ndani na nje ya Tanzania.
“Ni kweli tuna idadi kubwa ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu, Hatukurupuki kuongeza watu mikataba kama unavyoona malengo yetu sasa ni taji, hivyo kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi tunatakiwa kuwa na mastaa ambao watatubeba kwenye michuano hiyo.” Amesems Hersi Said
Wachezaji ambao wanamaliza mikataba mwisho wa msimu ni mabeki Bakari Mwamnyeto, Kibwana Shomari, Yassin Mustafa pamoja na viungo Zawadi Mauya, Deus Kaseke, Farid Mussa, Yacouba Sogne na Saido Ntibazonkiza.