Uongozi wa Young Africans umesema upo kwenye mpango mkakati wa kufanya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu pamoja na Michuano ya Kimataifa (Ligi ya Mabingwa Barani Afrika).
Young Africans imetangaza hatua hiyo, huku Ligi ya Msimu huu 2021/22 ikiendelea na timu yao inaongoza Msimamo kwa tofauti la alama kumi dhidi ya Mabingwa Watetezi Simba SC.
Mjumbe wa Kamati ya Usajili Young Africans Hersi Said amezungumza na Dar24 Media na kueleza mikakati ya klabu hiyo, huku akisema wamedhamiria kufanya usajili wa wachezaji ambao wataingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza na kuleta ushindani dhidi ya wachezaji waliopo.
“Unapofanya usajili ni lazima uwe na uhakika wa kumpata mchezaji ambaye ataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, sisi tumedhamiria kufanya hivyo ili kuwa na kikosi bora zaidi kwa msimu ujao.”
“Tumeshaanza kufuatilia baadhi ya wachezaji ambao wana hadhi ya kuichezea Young Afrcans, muda ukifika tutawatangaza hadharani, tuna uhakika wachezaji hawa watakua na tija kwenye kikosi chetu ambacho msimu ujao kitashiriki michuano ya Kimataifa.” amesema Heris Said
Kuhusu mipango ya kusaka taji la Ligi Kuu msimu huu Hersi amesema: “Mipango ya kuhakikisha tunatwaa ubingwa msimu huu bado tunaisimamia, tunaamini bado hatujafanikiwa lakini tunaendelea kuhakikisha hili linakwenda kama lilivyo sasa na kufikia lengo tunalolikusudia.”
Klabu ya Young Africans imekua na mabadiliko makubwa tangu ilipoanza kufadhiliwa na kudhaminiwa na Kampuni ya GSM, baada ya kuondoka kwa Mfadhili wao wa zamani Yusuph Manji, hali ambayo ilisababisha klabu hiyo kuyumba.