Rais wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Hersi Said amesema kila kitu kiko sawa kwa upande wa maandalizi ya mchezo wa Mkondo wa Pili hatua ya Mchujo Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kilichobaki ni wachezaji kutimiza wajibu wao.
Hersi ameyasema hayo kwenye mazoezi ya mwisho ya kikosi cha Young Africans yaliofanyika kwenye uwanja wa Olympic Rades uliopo Jiji la Tunis, Tunisia, ambao utatumika kwa mchezo leo Jumatano (Novemba 09).
Young Africans itashuka dimbani majira ya saa 2:00 usiku kwa saa za Tanzania, kupambana na Club Africain, ukiwa ni mchezo wa marudiano wa mchujo wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho BArani Afrika.
“Tunamshukuru Mungu maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia mia ikiwemo kuwahi mapema Tunisia kama alivyoshauri kocha wetu, Nasreddine Nabi”
“Tulifika mapema na timu ilipata kambi tulivu ya siku tatu kule Sousse na tukahakikisha wanakaa sehemu nzuri sana hapa Tunis”
“Tumewapa kila kitu na sasa jukumu limebaki kwa wachezaji. Jana tulikuwa na kikao kirefu na wachezaji na tuliwaambia hakuna mtu anayeweza kutupa matokeo hapa Tunisia isipokuwa wao. Mashabiki na wanachama wa Yanga wanataka kuona timu yao ikisonga hatua inayofata. Ni lazima wakapambane. Ujumbe wetu kwao ni huo,”
Young Africans inapaswa kusaka ushindi ama sare yoyote ya mabao, ili kufanikisha lengo la kutinga Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.