Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Hersi Said amesema mipango na mikakati ya klabu hiyo msimu huu 2022/23, ni kuhakikisha wanatetea Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Young Africans tayari imeshatetea Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba SC 2-1, Jumamosi (Agosti 13) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Rais Hersi amesema dhamira yao ni kutaka kuendelea kufanya vizuri katika soka la ndani ya Tanzania na upande wa Kimataifa (Ligi ya Mabingwa Barani Afrika) wamedhamiria kutinga hatua ya Makundi.
Hata hivyo kiongozi huyo amesema, licha ya kujiwekea mipango na mikakati hiyo, bado wanatambua wana kazi kubwa ya kufanikisha walichojiwekea sambamba na kuwa imara kiuchumi
“Matarajio yetu mwaka huu kama Young Africans ni kubakisha makombe matatu, na kuipelekea klabu yetu kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, sio rahisi inahitaji kuwa na kikosi imara na uimala wa kiuchumi ili kuweza kufika unapopataka” amesema Hersi Said
Young Africans jana ilianza Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania iliyokua nyumbani Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Mchezo ujao Young Africans itacheza dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.