Wakiwa wanajiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Merrikh, Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Injinia Hersi Said amnechimba mkwara mzito kuwa kwa ubora wa kikosi walichonacho msimu huu, wanaitaka Rekodi mpya kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Young Africans Septemba 16, mwaka huu itashuka ugenini kuvaana na Al Merreikh ya Sudan katika Mchezo wa Mkondo wa Kwanza katika Uwanja wa Pele mjini igali, Rwanda, kabla ya kurudiana jijini Dar es salaam kwenye Uwanja wa Azam Complex mwishoni mwa mwezi huu.
Kuelekea mchezo huo kikosi cha Young Africans kinajivunia kasi yao ambapo wamefuzu hatua ya kwanza ya awali kwa ushindi mnono wa mabao 7-1 wakiwatoa ASAS kutokea nchini Djibouti, huku pia wakiwa na mwenendo bora kwenye Ligi Kuu Bara anbapo wanaongoza msimamo na pointi zao sita walizokusanya kwenye michezo miwili ya kwanza.
Msimu uliopita kikosi cha Young Africans kwenye mashindano ya Kimataifa walianzia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walitolewa hatua ya mtoano na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika ambapo walifanikiwa kumaliza washindi wa pili wa mashindano hayo.
Akizungumzia ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Hersi amesema: “Kikosi kinaendelea na maandalizi ya mwisho ya michezo hii ya hatua ya mtoano, msimu uliopita tuliondolewa katika hatua kama hii na timu kutoka Sudan hivyo tunafahamu michezo hii.
“Lakini kama uongozi malengo yetu ni kuhakikisha tunaandika Rekodi mpya katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ambavyo tuliandika katika mashindano ya Kombe la Shirikisho kwa kucheza fainali msimu uliopita.”