Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Eng. Hersi Said, amefunguka kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC, huku akiweka wazi ahadi alizopewa na Wachezaji wake.
Young Africans itakayokuwa mwenyeji katika mchezo huo uliopangwa kupigwa Jumapili (Oktoba 23), Uwanja wa Benjamin Mkapa, itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwafunga watani wao Simba SC kwenye mpambano wa Ngao wa Jamii uliofanyika Mwezi Agosti 2022.
Hersi amesema baada ya kuondolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Wachezaji wake wengi waliumizwa na kitendo hicho baada ya kuzungumza nao, huku wengine wakiomba radhi kwa kumuandikia ujumbe mfupi wa simu, kwa kilichotokea Sudan.
Amesema wengi wamemuahidi kuwa wapo tayari kuingia katika mchezo dhidi ya Simba SC wakiwa na nguvu mpya, ili kufanikisha zoezi la kurejesha furaha kwa Mashabiki na Wanachama wa Young Africans waliokerwa na matokeo ya kupoteza dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
“Hata wachezaji wameumizwa na wapo ambao nimezungumza nao na wengine hata kuandika ujumbe wa kuomba radhi na sasa wanajua kwamba wamewaangusha mashabiki wao lakini wanataka kutafuta nguvu mpya ya kurejesha imani yao na hii itaanzia mchezo wetu dhidi ya Simba SC”
“Hata sisi viongozi tunataka kuona tunarejesha furaha kwa Mashabiki na Wanachama wetu ambao kwa hakika hawakupendezwa na kilichotokea kwenye Michuano ya Kimataifa, tupo tayari kwa hilo na tumejiandaa kuhakikisha lengo la kuifunga Simba SC Jumapili (Oktoba 23) linatimia.” amesema Hersi
Young Africans inakwenda kukutana na Simba SC ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 13 sawa na Simba SC iliyo kileleni, lakini miamba hiyo imetofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.