Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya ufundi ya Young Africans Hersi Said amesema ni matusi kusema Klabu hiyo haina Kikosi kipana na kusisitiza kuwa wana kikosi kipana ndio maana ilifika hatua ya Fainali Kombe la Shirikisho.
Hersi ametoa kauli hiyo kufuatia wadau wengi wa soka nchini kuikebehi Young Africans, wakiilinganisha na Simba SC kwa kulinganisha ubora na upana wa vikosi.
Akizungumza baada ya mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho dhidi ya SImba SC uliochezwa jana Jumapili (Julai 25), Hersi alisema hawana budi kujipongeza kwa kuwa na kikosi kizuri ambacho kimepambana na kufika kwenye hatua ya fainali.
“Ukisema Young Africans haina kikosi kipana unatukosea sana, ni sawa na kututusi, lakini ukweli ni kwamba kikosi chetu ni bora na imara ambacho kimeonyesha ukomavu hadi kufika hatua hii.”
“Ninawaahidi Mashabiki na Wanachama tutaendelea kukiboresha kikosi chetu kwa kufanya usajili, ninaamini msimu ujao tutakuwa na kikosi imara zaidi na kuna kitu tutakipata mwisho wa msimu.” amesema Hersi.
Young Africans ambayo itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kimataifa, imemaliza msimu ikiambulia patupu, huku mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho yakienda kwa watani zao Simba SC.