Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya Serikali kuongeza bajeti ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2021/2022 yenye kiasi cha Shilingi Bilioni 570 iliyoweka historia katika taasisi hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kufunga Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia Jijini Dar es Salaam leo Julai 31, 2021 Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kuwa ongezeko la bajeti hiyo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali katika kusaidia Watanzania wahitaji.
Mkurugenzi Badru amesema katika bajeti hiyo yenye uwezo wa kusomesha wanafunzi 160,000, imewalenga wanafunzi wahitaji wanaotokea katika kaya zisizojiweza na hivyo kuwataka kuhakikisha kuwa wanakamilisha taratibu za maombi kama zilivyoanishwa katika mwongozo wa uombaji mikopo wa mwaka 2021/2022.
“Kwa mwaka jana bajeti yetu ilisomesha wanafunzi 55,000 wa mwaka wa kwanza na kwa mwaka huu tunaratajia kusomesha wanafunzi 62,000 hii ni idadi kubwa kwa mwaka huu, tunawaomba wanafunzi wahitaji kuhakikisha wanaomba kwa usahihi,” Amesema Badru.
Akizungumzia kuhusu hali ya urejeshaji Mikopo, Badru amesema kwa sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wanafunzi wanufaika kurejesha mikopo yao kwa hiari, hatua iliyotokana na Serikali kufuta tozo na adhabu mbalimbali zilizokuwepo awali.