Katibu mkuu wa shirikisho la soka barani Afrika (CAF), Hicham El Amrani ametangaza kujizulu nafasi yake ikiwa ni juma moja baada ya aliyekua rais wa shirikisho hilo Issa Hayatou kuanguka kwenye uchaguzi mkuu kwa kushindwa na Ahmad Ahmad.
El Amrani, alithibitisha taarifa za kujiuzulu kwake kupitia barua aliyoiandika huko CAF, na alisema leo jumatatu atakabidhi ofisi kwa uongozi mpya, japo hakusema sababu za kuondoka kwake.
“Kwa masikitiko makubwa ninawataarifu kuwa nimejiuzulu leo nafasi yangu kama katibu mkuu wa CAF, baada ya miaka minane niliyoitumikia kwenye Shirikisho la Soka la Afrika,” aliandika El Amrani katika barua yake.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 37, raia wa Morocco amekua katibu mkuu wa CAF kwa miaka sita iliyopita.
Hata hivyo imeanza kuhisiswa kuondoka kwa El Amrani, huenda kunasababishwa na sera za uongozi wa mpya wa CAF za kutaka kufanya mabadiliko ya kiutendaji ndani ya shirikisho hilo, hivyo baadhi ya watu ambao wanajiona hawawezi kuwa sehemu ya maazimio hayo wameanza kujiondoa wao wenyewe.