Meneja wa muda wa klabu ya Chelsea, Guus Hiddink hajakata tamaa kwa timu yake kushika nafasi za juu katika msimamo wa ligi kuu ya soka nchini England, licha ya kuendelea kujikanyaga katika nafasi za chini.

Hesabu za meneja huyo ni kuhakikisha anakiacha kikosi cha The Blues katika mikono salama ya kushiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2016-17.

Klabu hiyo ya Stanford Bridge hivi karibuni imekuwa katika mwenendo wa kuridhisha baada ya kufanikiwa kutopoteza mchezo mmoja miongoni mwa michezo mitano waliyocheza tangu kuwasili kwa Hiddink.

Hiddink amesema ushindi wao dhidi ya Crystal Palace, ulimpa matumaini makubwa na kuamini huenda kikosi chake kikawa na bahati ya kipekee ya kufanya vyema kwenye kipindi hiki cha mzunguuko wa pili wa msimu wa 2015-16.

“Kila mmoja anajua kwamba tuna wachezaji stadi lakini wakati mwingine timu baada ya kutawazwa mabingwa, hulegea,” alisema Mholanzi huyo.

“Nilipoanza tulisema ikiwezekana tupate nafasi ya kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya litakuwa jambo zuri sana. Ni vigumu kwa sababu Ligi imekuwa na ushindani sana.

Kila timu inaweza kushinda nyingine. Hii inaifanya iwe vigumu kufika huko (nne bora). “Lakini tukiendelea kucheza kama leo tunaweza kuwa na furaha na tutaanza kupata matokeo mazuri. Bado inawezekana, ingawa bado kuna kibarua.”

Hiddink alipewa kazi ya ukufunzi baada ya Mreno Jose Mourinho kutupiwa virago.

Ronald Koeman: Wanyama Ataendelea Kuwa Mali Ya Southampton
Viongozi Wa Man Utd Wamuongezea Kiburi Louis Van Gaal