Serikali imeendelea kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ndani na nje ya nchi, ikilenga kuwavutia Watalii na Wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali Duniani, kupitia maonesho na matamasha kwa njia ya kidijitali.
Kauli hiyo imesemwa hii leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakati akijibu swali la Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.
Amesema, “Hifadhi hiyo imekuwa ikitangazwa katika matamasha mbalimbali ya Karibu Kusini, Kilifair na Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba na Nanenane na kwa njia ya kidigitali, mitandao ya kijamii, majarida na Safari Channel.”
Naibu Waziri Masanja ameongeza kuwa, Serikali imeanza kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi hiyo, ikiwemo kufanya ujenzi wa nyumba tatu za malazi ya Watalii na pia inatarajia kujenga nyumba mbili na kambi moja ya kuweka hema katika mwaka wa fedha 2023/2024, pamoja na kukarabati miundombinu ya barabara.
Kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka kati ya hifadhi hiyo na Wananchi, amesema tathmini ilishafanyika na kulielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA, kwa kuweka vigingi katika maeneo yaliyoainishwa.