Washambuliaji kutoka nchini Argentina wanaocheza soka katika ligi ya Italia (Serie A) Lautaro Martinez na Giovanni Simeone wametajwa katika kikosi cha wachezaji 20 cha nchi hiyo, tayari kwa michezo ya kimataifa ya kirafiki itakayochezwa mwanzoni mwa mwezi Septemba dhidi ya Guatemala na Colombia.
Taarifa iliyotolewa na chama cha soka nchini Argentina (AFA) imeeleza kuwa, washambuliaji hao wawili wameitwa katika kikosi hicho ambacho kinaongozwa kwa muda na makocha wazawa Lionel Scaloni na Pablo Aimar.
Martinez, ambaye alijiunga na Inter Milan akitokea Racing mwanzoni mwa msimu wa usajili wa majira ya kiangazi na Simeone ambaye ni mzaliwa wa Hispania anaeitumikia klabu ya Fiorentina, watacheza katika kikosi hicho kwa kushirikiana na washambuliaji wengine walioitwa kikosini Paolo Dybala, Angel Correa na Cristian Pavon.
Mshambuliaji wa Inter Milan Mauro Icardi ambaye aliachwa dakika za mwisho kabla ya safari ya kwenda Urusi kushiriki fainali za kombe la dunia, amerejeshwa kwenye kikosi hicho, huku Gonzalo Higuain, Sergio Aguero na Angel Di Maria wakitemwa.
Lautaro Martinez
Nahodha Lionel Messi naye hatokuwepo katika michezo hiyo miwili ya kimataifa ya kirafiki, baada ya kuomba asiitwe kikosini kwa maamuzi yake binafsi, ambapo inaelezwa mshambuliaji huyo wa FC Barcelona anahitaji kupumzika katika kipindi chote kilichosalia kwa mwaka huu 2018, na huenda akarejea tena katika timu ya taifa mwanzoni mwa mwaka 2019.
Ni wachezaji tisa pekee ambao walikua miongoni mwa wachezaji 23 walioshiriki fainali za kombe la dunia nchini Urusi, walioitwa kwenye kikosi ambacho kitaingia kambini mapema mwezi ujao kabla ya kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Guatemala mjini Los Angeles (USA) Septemba 07 na siku nne baadae kitapambana na Colombia mjini New Jersey (USA).
Kiungo wa klabu ya Sevilla Franco Martinez, ambaye aliichezea timu ya taifa ya Argentina kwa mara ya kwanza mwaka 2015 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Italia, naye amejumuishwa kwenye kikosi hicho sambamba na beki wa klabu ya Gremio Walter Kannemann.
Makocha wa muda wa kikosi cha Argentina Lionel Scaloni na Pablo Aimar, pia wamemuita kiungo wa klabu ya Stuttgart ya Ujerumani Santiago Ascacibar na mlinda mlango wa Real Sociedad Gerónimo Rulli.
Giovanni Simeone
Kikosi cha Argentina kimekua na mabadiliko makubwa ya wachezaji, baada ya nchi hiyo kufanya vibaya kwenye fainali za kombe la dunia nchini Urusi, ambapo kililazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Iceland kabla ya kufungwa na Croatia huku kikiifunga Nigeria katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi.
Katika hatua ya 16 bora, Argentina walikwaa kisiki cha mabingwa wa dunia Ufaransa kwa kukubali bakora nne kwa tatu na kutupwa nje ya fainali hizo zilizoanza Juni 14 na kufikia tamati Julai 15 mjini Moscow.
Kikosi kamili kilichoitwa kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Guatemala na Colombia upande wa Makipa: Franco Armani (River), Geronimo Rulli (Real Sociedad) na Sergio Romero (Manchester United).
Mabeki: Fabricio Bustos (Independiente), Gabriel Mercado (Sevilla), German Pezzella (Fiorentina), Ramiro Funes Mori (Villarreal), Alan Franco (Independiente), Nicolas Tagliafico (Ajax), Walter Kannemann (Gremio), Leonel Di Plácido (Lanus), Eduardo Salvio (Benfica) na Marcos Acuna (Sporting Lisbon).
Viungo: Leandro Paredes (Zenit), Santiago Ascacibar (Stuttgart), Rodrigo Battaglia (Sporting Lisbon), Gonzalo Martinez (River), Giovani Lo Celso (PSG), Franco Cervi (Benfica), Maxi Meza(Independiente), Matias Vargas (Velez), Franco Vazquez (Sevilla) na Exequiel Palacios (River).
Washambuliaji: Angel Correa (Athletico Madrid), Lautaro Martinez (Internazionale), Mauro Icardi (Internazionale), Giovanni Simeone (Fiorentina), Cristian Pavon (Boca Juniors) na Paulo Dybala(Juventus).