Rekodi za Mshambualiji mpya wa Simba SC Pa Omar Jobe, raia wa Gambia zimeonesha kuwa amefunga mabao 41 katika mechi 73, akichezea klabu tano tofauti.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amejiunga na Simba SC kwa mkataba wa miaka miwili akitokea katika Klabu ya FC Zhenis ya Kazakhstan.

Usajili huo umekamilishwa baada ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha kulalamika kuwa kwa sasa anakosa mshambuliaji mwenye uwezo wa kupachika mabao na mwenye nguvu ya kukabiliana na mabeki wababe ndani ya eneo la hatari.

Rekodi zinaonesha kuwa Jobe alifunga mabao 23 na ‘asisti’ tano, katika mechi 28 kwenye Ligi Kuu ya Bangladesh. Katika Ligi Kuu ya Kazakhstan akifunga mabao 13 na ‘asisti tano katika michezo 25 aliyocheza.

Jobe akiwa katika Ligi Kuu ya Macedonia Kaskazini alifunga mabao matatu katika mechi 12 wakati kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kutua timu hiyo ya Ulaya alifunga mabao mawili katika mechi nne huku Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa hajaziona nyavu katika michezo miwili aliyocheza.

Katika maisha yake ya soka, klabu alizozichezea Jobe ni pamoja na Shkendija na Struga za nchini Macedonia, msimu wa 2022/23 alijiunga na Klabu ya Neman Grodno ya nchini Beralus kabla ya kujiunga na Zhenis na sasa Simba SC.

Kabla ya hapo, Mgambia huyo alianza kuzichezea Klabu za Tallinding United FC ya nchini mwao, 2011 hadi 2014, alitimkia kwenye Klabu ya ASEC Ndiambour ya Senegal, 2017 hadi 2019 alicheza michuano ya Afrika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Akizungumza wakati akitambulishwa Simba, Jobe hakuwa na maneno.mengi zaidi ya kusema “nipo hapa kwa ajili ya kufunga mabao”.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Salim Abdallah “Try Again’, amesema wameongeza mchezaji mwingine wa nafasi hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu na kuwasukuma waliopo ili waweze kufanya vizuri.

Tumeongeza mchezaji mwingine wa nafasi ya ushambuliaji kuja kuongeza nguvu katika eneo hilo tunamkaribisha sana Jobe,” amesema Try Again.

Hata hivyo, kusajiliwa kwa Mshambuliaji huyo kutafanya safu ya ushambuliaji ya Simba SC kuwa na Washambuliaji wanne, na kumpa wigo mpaka kocha, ambapo kwa sasa ina nahodha John Bocco, Jean Baleke na Moses Phiri.

Kwa siku za karibuni, mastraika hao wote wameonekana kutokuwa kwenye kiwango chao cha kawaida kiasi cha kumfanya Benchikha kulalamika kupatiwa Mshambuliaji mwingine haraka.

Wakati huo huo, Klabu ya Simba SC imesema kocha wao Benchikha ameonekana kufurahishwa na michuano ya Kombe la Mapinduzi kwani imempa nafasi ya kujua mchezaji gani wa kubaki na wakuondoa yeye mwenyewe bila kuambiwa na mtu.

 

Benchikha achekelea usajili Simba SC
Tishio la Mahakama: Muhubiri tata Mackenzie ashitakiwa rasmi