Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Job Ndugai amesema kuwa kitendo cha viongozi wa umma kuhujumu uchumi wa nchi ni kitendo kisichofaa kwenye jamii, pia ni laana kwa viongozi hao.

Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kukabidhi ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini aina ya Almasi na Tanzanite Ikulu, ambapo amesema ni aibu kwa viongozi wa umma kutafuna mali za umma.

Amesema kuwa kama watu hao wangekuwa wanaguswa na umasikini na matatizo yanayowakabili wananchi ambao ni Watanzania wenzao wasingeweza kuhujumu uchumi wa nchi.

“Ni ukweli usiopingika kwa sisi ambao ni wabunge kutoka vijijni unapozunguka jimboni kwako kule kijijini inafikia kipindi unajiuliza hivi hawa wananchi nitafanyaje hapa angalau pasogee kidogo, unakuta watoto waliokaa chini mpaka unapatwa na uchungu,”amesema Ndugai

Aidha, ameongeza kuwa wanamshukuru Rais sasa Dkt. John Magufuli kwa sera zake nzuri ambazo zimeweza kusaidia watoto wa shule angalau wanakaa kwenye madawati kwa juhudi zake na msukumo alioweka.

Hata hivyo, Ndugai ameonyesha kushangazwa na watu hao ambao mara nyingi wamekuwa wakitajwa kwenye matukio ya kuhujumu uchumi, kuendelea kuwepo bungeni kwa kuendelea kuchaguliwa na wananchi wao, licha ya matendo yao machafu kwa nchi.

Magazeti ya Tanzania leo Septemba 8, 2017
CCM walaani tukio la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu