Msichana wa Nigeria amezua gumzo baada ya kuzuiwa kuingia ukumbini kwenye sherehe za kutunukiwa shahada yake (graduation) kwa kuwa alikataa kuvua vazi linalofunika kichwa chake linaloitwa ‘hijab’.
Msichana huyo aliyetajwa kwa jina la Amasa Firdaus alikutwa na mkasa huo nje ya ukumbi wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Ilorin ambapo sherehe hizo zilikuwa zinafanyika.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, waratibu wa sherehe hizo walimzuia kuingia kwenye ukumbi huo kwa madai kuwa vazi hilo halikuwa kwenye utaratibu wa mavazi yaliyokubaliwa (dress code).
Uamuzi huo uliibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutua kwa mara ya kwanza kwenye mtandao wa Instagram, wengi wakiulaani kwa madai kuwa ulikiuka haki yake.
Hata hivyo, baadhi ya watu walitetea uamuzi wa chuo hicho wakieleza kuwa Amasa alipaswa kuheshimu taratibu za chuo kilichoko Lagos.