Nahodha wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, anatarajiwa kuelekea jijini Cape Town, nchini Afrika Kusini, kesho Alhamisi kufanyiwa uchunguzi wa goti la mguu wake kulia linalomsumbua.

Ninja ambaye amekosa takribani mechi nne zilizopita za Azam FC baada ya kupewa mapumziko maalum kupisha matibabu ya tatizo hilo, amekuwa nguzo muhimu ya timu hiyo na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika eneo la kiungo cha ukabaji na baadhi ya mechi akitumika kama beki wa kulia.

Daktari Mkuu wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Nahodha huyo Msaidizi wa Stars atafanyiwa uchunguzi huo katika Hospitali ya Vincent Pallotti mjini humo ili kujua undani wa tatizo lake huku akidai ataanza kuchukuliwa vipimo na Dr. Nickolas Ijumaa hii.

“Himid amekuwa akicheza na maumivu makali katika goti la kulia na tulimzuia kucheza mechi baada ya mechi mbili zilizoita baada ya kuona yale maumivu yanaendelea na tulifanya vipimo vya M.R.I ambavyo vilionyesha kuna hitilafu kwenye goti lake na alipata matibabu katika Hospitali ya Moi (Muhimbili).

“Lakini baada ya kupata matibabu takribani wiki moja tuliamua ni busara zaidi kumpeleka katika Hospitali ya Vincent Pallotti nchini Afrika Kusini kwenda kuangaliwa zaidi ukiangalia Himid bado ana majukumu ya klabu na makubwa ya timu ya Taifa vilevile kama nahodha,” alisema.

Young Africans yaikandamiza Majimaji FC uwanja wa Taifa
Fuvu la kichwa lamuweka pembeni Ryan Mason