Kocha mkuu wa Klabu ya Namungo FC ya Lindi, Thiery Hitimana amesema yuko tayari kumsajili mshambuliaji Raia wa Zimbabwe Donald Ndombo Ngoma, aliyeachwa na Azam FC baada ya mkataba wake kufikia kikomo.
Hitimana amesema umbo la Ngoma linamshawishi kumhitaji kwenye kikosi chake, pia rekodi yake huko nyuma akiwa Young Africans na Azam FC inaonesha ni mchezaji mzuri.
Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema suala la kumsajili mshambuliaji huyo, litategemea na makubaliano kati yake na uongozi wa Namungo FC ambao umedhamiria kukiboresha kikosi chao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara.
“Ninapendezwa sana na uchezaji wake, ana umbo zuri na nina imani kama nitafanikiwa kumsajili atatusaidia sana katika kikosi chetu msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.”
“Umbo la Ngoma linamshawishi kumhitaji kwenye kikosi chake pia rekodi yake huko nyuma akiwa Young Africans na Azam FC inaonesha ni mchezaji mzuri.” Amesema kocha Hitimana.
Azam FC ilithibitisha kuachana na Donald Ngoma Juni 14, kufuatia mkataba wa pande hizo mbili ulioanza rasmi mwaka 2018 kufikia kikomo.
Kwa kipindi chote cha misimu miwili, alichodumu ya Azam FC, Ngoma amekuwa mmoja ya washambuliaji wa kutumainiwa akiwa mfungaji bora msimu uliopita wa Azam FC kwa mabao yake 14 aliyoifunga kwenye mashindano yote.
Hadi anamaliza mkataba wake kwenye timu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Ngoma amefanikiwa kucheza jumla ya mechi 42 za mashindano yote, akihusika katika mabao 20, baada ya kufunga 16 na kutoa pasi za mwisho nne.