Aliyekua Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Thiery Hitimana amesema yupo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Kocha Mpya wa klabu hiyo Franco Pablo Martin, ambaye anatarajiwa kutua nchini wakati wowote juma hili.
Kocha Fanco alitajwa kushinda nafasi ya kuwa Kocha Mkuu Simba SC, Jumamosi (Novemba 06) Usiku, akiwapiku makocha wengine zaidi ya 50 walioomba nafasi ndani ya klabu hiyo, baada ya kuondoka kwa Didier Gomes mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Hitimana amesema anajua wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanarejea kwenye ubora wao hivyo hatosita kumpa ushirikiao kocha Franco, ili kufanikisha lengo linalokusudiwa na kutarajiwa na familia ya klabu ya SImba SC.
“Suala la kocha mpya kwangu siyo shida kwa sababu maisha ya mpira ndiyo yamekuwa hivyo siku zote, leo inaweza kuwa imekaa hivi lakini kesho unaweza kukuta mambo yapo tofauti lakini jambo la msingi ni kuangalia kwetu na kocha mpya nini ambacho tunaweza kukifanya katika michezo iliyo mbele yetu.”
“Najua ni kwamba nitamwambia au kumpa ripoti ya michezo ambayo tumeshacheza na ile ambayo hatujacheza ili kuweka mikakati ya kupata matokeo, tuna michezo miwili ya Kombe la Shirikisho ambayo inahitaji mikakati, na ule dhidi ya Young Africans ili kuweza kujua tunapitia wapi, kucheza na Young Africans ni presha kubwa hivyo mwalimu lazima apate nafasi ya kuwajua kwa kuwaangalia na kumwambia,” amesema Hitimana.
Ligi Kuu Tanzania Bara itakaporejea baada ya kupisha michezo ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022, Simba SC itakua mgeni wa Ruvu Shooting Uwanja wa Benjamin Mkapa, na huenda Kocha Franco Pablo Martin akawa sehemu ya benchi la ufundi siku hiyo.
Simba SC inashika nafasi ya pili katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 11, zilizotokana na ushindi katika mchezo mitatu dhidi ya Dodoma Jiji FC, Polisi Tanzania na Namungo FC, huku ikitoa sare dhidi ya Coastal Union na Biashara United Mara.