Hatimae uongozi wa Namungo FC umesitisha mkataba wa kocha Hitimana Thiery, baada ya pande hizo mbili kufanya mazungumzo na kukubaliana.

Kocha Hitimana ambaye aliisaidia Namungo FC kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita kwa mara ya kwanza, anaondoka klabuni hapo huku tetesi zikieleza huenda nafasi yake ikachukuliwa na kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), Hemed Morocco.

Taarifa rasmi ya kusitishwa mkataba wa kocha huyo kutoka nchini Burundi zimetolewa kwenye mitandao ya kijamii ya klabu ya Namungo FC.

“Kwaheri kocha Thiery Hitimana, tunatambua na kuthamini mchango wako kwenye timu yetu 2018/2020. Tunakutakia kila la heri na mafanikio.” Ni ujumbe ulioandikwa kwenye ukurasa wa Instagram wa klabu ya Namungo FC.

Mbali na kuipandisha Ligi Kuu Tanzania Bara Namungo FC, kocha Hitimana Thiery ameiwezesha klabu hiyo kushiriki michuano ya Kombe La Shirikisho Barani Afrika (CAF).

Mchezo wa kwanza wa Kombe La Shirikisho Afrika kwa Namungo FC utawakutanisha dhidi ya Al Rabita FC ya Sudan Kusini.

Namungo FC walipata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe La Shirikisho Afrika baada ya kuwa mshindi wa pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC), wakifungwa na Simba SC katika mchezo wa fainali uliochezwa mkoani Sumbawanga mwezi Agosti.

Hili hapa Baraza jipya la Mawaziri Zanzibar
Gwajima: Namhitaji Halima Mdee, sitamuacha (Exclusive-Video)