Siku moja baada ya kutambulishwa kama kocha msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, wasifu wa Kocha Hitimana Thiery umeanikwa hadharani kwa kuthibitisha vigezo ambavyo vinakidhi katika soka la Tanzania na Kimataifa.
Hitimana alitambulishwa kuwa kocha msaidizi wa Simba SC jana Ijumaa (Septemba 10) majira ya jioni, baada ya kuibuka kwa mkanganyiko wa kigezo cha elimu ya Kocha Mkuu Didier Gomez, ambaye amepigwa stop na Shirikisho la soka Barani Afrika CAF.
Kocha Hitimana kumbe ana elimu ya kutosha kwenye soka na hata nje ya mpira kwani ana Leseni A ya Shirikisho la Soka Barani Africa (CAF).
Pia Kocha huyo kutoka nchini Rwanda, pia ni Mkufunzi wa Makocha anayetambuliwa na CAF, na nje ya Soka ana Shahada ya Biashara na Shahada ya Uzamili (Masters) kwenye Utawala.
Katika uzoefu wake amefundisha timu mbali mbali na kuwatoa wachezaji wengi wanaotamba kwenye soka la ushindani akiwamo Haruna Niyonzima aliyewahi kuzitumikia klabu kongwe nchini za Simba SC na Young Africans na Meddie Kagere wa Simba SC.
Timu alizowahi kufundisha ni Rayon Sports mwaka msimu wa 2003/4 na kipindi hicho, alikuwa akiwanoa wachezaji wengi akiwamo aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Simba SC, Masoud Djuma.
Pia msimu wa 2004/6, aliifundisha Light Stars Seychelle, ambapo katika kikosi chake walikuwamo, Bakari Malima, Peter Manyika na Djuma kabla ya kurudi Rayon msimu wa 2006/9 akiwano tena Djuma na Haruna Niyonzima, ambapo alikuwa akimsaidia Luc Eymael wa Young Africans kwa sasa.
Timu nyingine ni Musanze FC (2009/10), AS Kigali (2010/12).
Kwa nchini Tanzania amezinoa Namungo FC, Mtibwa Sugar na Biashara United Mara FC.