Kocha Mkuu wa KMC FC Thierry Hitimana ameivisha Ubingwa wa Tanzania Bara 2021/22 Young Africans, baada ya kikosi cha kukubali kichapo cha 2-0 katika mchezo wa Mzunguuko wa 18 uliopigwa Jumamosi (Machi 19) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Hitimana ametoa nafasi hiyo kwa Young Africans, baada ya kikosi chake kuangukia pua kwa kukubali kufungwa 2-0, na kutoa nafasi kwa vinara hao wa Msimamo wa Ligi Kuu kufikisha alama 48.
Hitimana amesema : “Young Africans ni timu ambayo inapata matokeo mazuri kwa kila mechi inayocheza kwa msimu huu, sisi tulikuwa na madhaifu kwa upande wa mabeki wetu, licha ya sisi kupata nafasi nyingi za kufunga ila tukakosa, inabidi kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao.”
“Kwa asilimia 80% Young Africans wana uwezo wa kuchukua ubingwa msimu huu kutokana na uwezo wao ndani na nje ya uwanja.”
Hitimana ameongeza kuwa msimamo wa ligi unatoa picha bingwa wa msimu huu nani.
“Lipo wazi kabisa hilo la ubingwa, kwa kifupi ni kuwa bingwa tayari ameshajulikana hadi hivi sasa, msimamo wa ligi unaonyesha.
“Tangu kuanza kwa ligi Young Africans imeonekana kucheza katika kiwango bora, imekuwa ikipata matokeo mazuri ya ushindi hata kama ikicheza kiwango kibovu.
“Kwetu sisi KMC tunapambania kumaliza ligi katika nafasi za katikati katika msimamo, lakini siyo ubingwa kwani tulikuwa na tatizo kubwa kwenye eneo la ulinzi na ndio maana tumepata shida kubwa, hatukuwa bora kwenye ulinzi na Young Africans wametuadhibu kwa hilo.”
Kwa kichapo cha 2-0 ilichokipokea kutoka kwa Young Africans, KMC FC imeendelea kubaki na alama zake 22 zinazoiweka katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.