Kampuni ya Promosheni ya ngumi za kulipwa nchini, Mitra Boxing Promotion imefunguka sababu kubwa iliopelekea kupeleka pambano la bondia Karim Mandonga mkoani Dodoma ni kutaka kuongeza chachu ya mchezo huo kwa kuhakikisha vipaji vinaendelezwa.
Kampuni hiyo imetoa kauli hiyo kuelekea katika pambano kubwa waliloliandaa ambalo linatarajia kupigwa Juni 24, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Chinangale Park, mkoani Dodoma huku likipewa jina la Kivumbi.
Mmoja kati ya watendaji wa kampuni hiyo, Chubert Mwarabu amekiambia Kijiwe cha Ndondi kuwa malengo yao makubwa ni kuleta chachu na kuchachua mchezo huo kwa kuhakikisha wanaibua vipaji vipya katika mchezo wa ngumi za kulipwa na kuendeleza vipaji vilivyokuwepo.
“Malengo yetu kama kampuni ni kuleta chachu na kuchachua mchezo wa ngumi nchini, kuibua vipaji vipya kuendeleza na kukuza vile ambavyo vimekwisha kuonekana, hamasa na kiwango cha watu wanaofuatilia imekuwa kubwa kila kukicha.”
“Mitra Boxing Promotion tumeichagua Dodoma katika pambano letu linalotarajia kupigwa Juni 24, mwaka huu ambapo bondia wetu, Mtanzania mwenzetu Karim Mandonga atapanda ulingoni dhidi ya Charles Misanjo kutoka Malawi, litakuwa ni pambano la kipekee kutokana na fursa zilizopo hapa Dodoma na nguvu ya serikali yenyewe ipo hapa Dodoma.” amesema Mwarabu