Makamu mwenyekiti wa klabu bingwa Tanzania bara Young Africans, Clement Sanga, amefunguka na kuweka wazi sababu za uongozi kutomsajili winga wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Khalfan Ngassa.
Sanga alisema alishangazwa na taarifa zilizoenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii mwishoni mwa juma lililopita, zikidai kuwa, Young Africans wamemrudisha Ngassa katika kikosi chao.
Alisema ilikuwa ni vigumu kumsajili Ngassa kwani katika ripoti ya msimu uliopita ya kocha Lwandamina, hakuna sehemu aliyopendekeza winga huyo asajiliwe.
“Hakuna ukweli wowote kuhusu Ngassa kusajiliwa na Young Africans, kwa ufupi klabu yetu haimuhitaji Ngassa na hakuwepo katika mapendekezo ya kocha George Lwandamina,” Alisema Sanga.
“Hatuwezi kumsajili mchezaji ambaye hakuwepo katika mipango ya mwalimu, hivyo tumesajili kulingana na matakwa ya kocha na si mtu mwingine, kwa hiyo Ngassa hakuwa na nafasi,” aliongeza Sanga.
Kwa muda mrefu Ngassa amekuwa na shauku kubwa ya kutaka kurejea katika kikosi cha Young Africans licha ya kushindwa kufanya vizuri akiwa na kikosi cha Mbeya City na Free State ya nchini Afrika Kusini.