Polisi wenye silaha nchini Kenya, wameweka vizuizi kwenye barabara zinazoelekea Ikulu jijini Nairobi huku kukiwa na hofu ya maandamano ya wapinzani yaliyokuwa yamepangwa ambapo Madereva wa magari wamekuwa wakizuiwa na kupekuliwa katika sehemu mbalimbali barabarani.
Hatua hiyo inafuatia tangazo la upinzani lililotolewa hivi karibuni juu ya kuandamana kupinga kupanda kwa gharama za maisha na kuituhumu Serikali kushindwa kushughulikia machungu ya gharama hizo za kwenye maisha ya kawaida.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amekuwa akifanya mikutano ya kuipinga serikali nchini humo, akisema imeshindwa kumtambua Mkenya wa hali ya chini na kwamba upandaji wa bei za mafuta na bidhaa za vyakula unamkandamiza Mwananchi wakati viongozi wakiwa na uhakika wa pato na chakula.
Hata hivyo, Rais wa Kenya, William Ruto amekuwa akisisitiza kuwa hatamuonea haya wala kusita kumchukulia hatua yeyote atakayekiuka taratibu za kisheria au kutishia amani ya Wakenya na kwamba Serikali yake inamjali kila mpiga kura.