Mshambuliaji kutoka nchini England Eddie Nketiah ameingiwa na hofu kuhusu hatima yake ndani ya Arsenal kutokana na ujio wa Kai Havertz, gazeti la The Sun limefichua.
Nketiah mwenye umri wa miaka 24, alikuwa sehemu ya kikosi cha Mikel Arteta msimu uliopita baada ya Gabriel Jesus kukaa nje kwa muda mrefu alipoumia goti.
Nketiah alifunga mabao manane na kutengeneza asisti tatu katika mechi 39 alizocheza msimu uliopita. Lakini baada ya Arsenal kumsajili Havertz, fowadi huyo amepata presha anaweza kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza msimu ujao.
Sasa timu kama West Ham, Crystal Palace na Fulham zinafumfuatilia na chochote kitakachotokea kuhusu hatima ya Nketiah basi watapigana vikumbo kuwania saini yake.
Chanzo cha habari kimeripoti: “Eddie anafikiria hatima yake kwa sasa, anadhani amefikia kiwango kikubwa na anataka kucheza kila wiki, sasa mambo yatamuendea magumu kutokana ujio wa Havertz, anaweza akafosi kuondoka, West Ham na Crystal Palace zinamtolea macho.”
Gazeti la Sun Sports linaelewa Arsenal haina mpango wa kumfosi Nketiah aondoke kwasasa Arteta anatambua uwezo wake.
“Mikel Arteta anatambua uwezo wa Nketiah, baada ya kurejea UEFA nadhani anafikiria kuwa na mastraika watatu ndio maana akamsajili Havertz, Arteta anaweza akachezesha mastraika wawili msimu ujao kutokana ma mabadiliko hayo.”