Kundi la paka wapatao 12 wameshiriki mazishi ya Salehe Matiko aliyezikwa saa 10 alasiri ya Agosti 24 katika Kijiji cha Chikalala mkoani Lindi.

Marehemu Matiko aliuawa kwa kushambuliwa na wakazi wa kijiji hicho kwa tuhuma za ushirikina huku akidaiwa kuwatesa watu ikiwa ni pamoja na kuua ndugu zake.

Wananchi wa kijiji hicho walieleza kuchoshwa na kile walichokiita mateso ya Matiko na kuamua kumuwinda na kumshambulia mpaka kupoteza maisha yake.

Wakiwa msibani baada ya taratibu zote za kuandaa safari yake ya mwisho, jeneza lake lilibebwa kwa utaratibu wa kawaida lakini ghafla wakiwa barabarani kuelekea makaburini liliibuka kundi la paka lililokuwa likifuata jeneza hilo kwa nyuma hali iliyoibua hofu kwa wanakijiji.

Lakini paka hao walifika hadi makaburini ambapo nao walishiriki mazishi yake.

Wakati wa kushusha maiti kwenye kaburi lake, paka hao waliinamisha vichwa chini wakionesha utii wao kwa marehemu jambo ambalo liliwashtua wengi.

Baada ya kumaliza taratibu zote za kumuhifadhi Matiko watu walioshiriki mazishi hao walitawanyika kama ilivyo ada lakini paka hao hawakutawanyika na badala yake waliendelea kubaki makaburini hapo.

Msafiri Msemwa ambaye ni mkazi wa kijiji hicho ameeleza kuwa, waliingia hofu kidogo kwa kuwa sio tukio la kawaida lakini waliendelea na taratibu za mazishi hayo.

“Sio jambo la kawaida kutokea ndio maana kila mmoja alikuwa na hofu lakini watu waliendelea kama kawaida mpaka mwisho.

“Kila mmoja alikuwa na tafsiri yake kutokana na kundi hilo la paka ambapo muda wote wa mazishi watu walikuwa wakiwatolea macho paka hao huku wakichukua tahadhari kwa lolote ambalo lingeweza kutokea,” amesema

Nacer Chadli atimkia Ufaransa
Afisa Elimu, Mkuu wa shule kibeta wasimamishwa kazi