Kufuatia kukamatwa kwa zaidi ya bunduki 200 na risasi 3,000 eneo la Kaunti ya Marsabit baada ya operesheni ya usalama inayoendelea nchini Kenya, wakazi wa eneo hilo wamehimizana kutafuta amani badala ya kutupiana lawama juu ya uwepo wa silaha hizo.
Wakiongea katika eneo hilo, wakazi hao wamedai vitendo vya kutupiana lawama havitasaidia na vinaleta ishara mbaya kwani lengo ni usalama kwanza na si kutengeneza mazingira ya kuanzisha ugomvi baina yao utakaosababisha machafuko yasiyo ya lazima na kuleta hasara katika familia.
Mmmoja wa wakazi wa eneo hilo James Okoth pia amezitaka mamlaka za Serikali kuweka utaratibu wa ulinzi utakaosaidia kutuliza ghasia zinazoweza kujitokeza iwapo Polisi itaondoa doria yake katika eneo hilo na kwamba elimu inatakiwa juu ya madhara ya kumiliki silaha kiholela.
”Kuna hatari hapa maana watu wanakamatana uchawi hapa hii haitasaidia cha muhimu ni kujenga umoja na kutafuta amani baina yetu maana silaha hizi ni hatarishi na zinaweza kutudhuru niombe mamlaka kutusaidia kuelimisha madhara ya umiliki wa silaha kiholela,” amesisitiza Okoth.
Juni 6, 2022 Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang’i alisema wataendelea na zoezi la kukamata silaha na kupiga kambi katika eneo la Rapid Deployment Unit (RDU), lililopo Marsabit nchini humo hadi pale watakapojiridhisha kuwa amani imepatikana.
“Tutasalia katika eneo hili hadi amani itakapopatikana na tumetoa hakikisho kwamba hatutamaliza operesheni hii mpaka baada ya uchaguzi mkuu kwa sababu tunataka mahali hapa pawe salama,” amesema.
Marsabit, ambayo imekuwa na matukio ya mara kwa mara ya machafuko imekuwa chini ya amri ya kutotoka nje tangu Mei 2, 2022 huku biashara haramu ya bunduki na wizi wa ng’ombe ikikithiri katika eneo hilo, na kusababisha serikali kuingilia kati.
Matiang’i, hata hivyo, amesema Serikali itapitia upya wazo lake la saa za kutotoka nje, ili kuruhusu wafanyabiashara kufanya kazi kikamilifu, huku tukio hili likijiri wakati ambao Kenya inatafakari kuongeza muda wa kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi wakati wa uchaguzi mkuu.
“Tutakagua saa za kutotoka nje katika muda wa wiki tatu hadi nne na tunalenga kurejesha angalau bunduki 5,000 kutoka kwa wamiliki haramu ” amesema.
Hata hivyo, Waziri huyo alionyesha kufadhaika kutokana na afisa wa zamani wa jeshi kuwa ndiye mshukiwa mkuu wa ulanguzi wa silaha haramu mjini Marsabit ambaye aliachiliwa na Mahakama ya sheria kufuatia kukamatwa kwake.
“Nimesikitishwa sana kuhusu jinsi mtu huyo alivyoachiliwa kupitia mfumo wa haki kwa njia ambayo sio ya kuvutia kwetu tunarudi Mahakamani kukata rufaa kwa sababu tuna ushahidi wa kutosha wa kumshtaki mtu huyo,” amesisitiza.
Zoezi la ukamataji wa silaha hilo linaendeshwa kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali, ambapo katika msafara huo Waziri huyo aliandamana na inspekta mkuu wa polisi nchini Kenya Hillary Mutyambai na maafisa wengine wakuu wa usalama.