Chama cha waandishi wa habari nchini Uganda kinalaani ongezeko la ukamataji kiholela waandishi nchini humo unaofanywa na Jeshi la Polisi kisha kufunguliwa kesi za uhaini na wengine kutekwa na watu wasiojulikana kisha kupelekwa magerezani bila kufikishwa mahakamani.
Taarifa hiyo iliyotolewa baada ya waandishi wa habari watatu wa gazeti la Daily Monitor kukamatwa katika mazingira ya kutatanisha na kushtakiwa kwa njama ya kujaribu kuipindua serikali, mashtaka ambayo adhabu yake ni kifo endapo watakutwa na hatia.
Uganda kumekuwa na ripoti za waandishi wa habari kutekwa na watu wasiojulikana kisha baadaye kupatikana gerezani wakiwa wamefungwa bila hatia kumezua hofu kubwa kwa waandishi wa habari.
Jana Februari 19, 2018 mwandishi wa habari wa kituo cha binafsi cha habari cha Top Radio, Richard Kasule alikamatwa nje ya ofisi za kituo hicho muda mfupi baada ya kuandaa matangazo ya asubuhi.
-
TRA yatoa matokeo ya uchunguzi uliofanywa kwa Askofu Kakobe, na kubaini haya
-
Mambosasa aagiza vigogo 7 wa Chadema kuwekwa chini ya ulinzi
Wafanyakazi wenzake katika kituo hicho cha habari walidai kwamba Kasule alikamatwa na polisi baada ya kufichua ushirikiano kati ya walinda usalama na makundi ya uhalifu jijini Kampala baada ya kufanya mahojiano na viongozi wa makundi ya uhalifu walioshirikiana na polisi katika uhalifu huo.
Hatua ya kukamatwa kwa kasule inajiri siku mbili baada ya mwandishi wa gazeti la serikali la the New Vision, Charles Etukuri, kukamatwa nje ya ofisi za gazeti hilo la serikali.
Etukuri alichapisha taarifa ya upekuzi kuhusiana na kifo cha muwekezaji kutoka bara la Ulaya katika hoteli moja maarufu jijini Kampala, na kukamatwa kwa viongozi wakuu 6 wa polisi kisiri.
Mwandishi mwingine wa habari, Isaac Bakka, alipatikana gerezani baada ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha wiki mbili zilizopita.
Hata hivyo, Mahakama jijini Kampala kupitia Mkurugenzi wa Habari, Solomon Muyita, amesema mwandishi huyo alikuwa amefunguliwa mashtaka ya uagizaji wa silaha hatari kwa nia ya kuipindua serikali ya Yoweri Museveni.
Wahariri wa gazeti la upekuzi la Red Pepper, Juice FM na gazeti linalochapishwa kwa lugha ya kiganda la ‘Kamunye,’ nao wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuipindua serikali ya rais Yoweri Museveni.
Vituo hivyo vimefunguliwa hivi majuzi baada ya kufungiwa kwa mda wa mwezi mmoja kwa makosa ya kuandika habari za kichochezi na zenye lengo la kuvuruga amani nchini humo.