Na Zitto Kabwe
Kwamba Mashirika ya umma nchini yanamkabidhi Rais cheki za magawio (dividends) ya faida zao ni ama Ofisi ya Rais inafanya Siasa au hawajui maana ya gawio.
Tukiwa Bunge la 9, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC na baadaye PAC) ililishauri Bunge kufanya marekebisho ya Sheria ya baadhi ya mashirika ya umma Ili kiwango fulani cha Mapato ghafi (turnover) kitolewe Serikalini kama maduhuli ya Serikali.
Serikali ya wakati huo ilikubali na Sheria zikabadilishwa na kutenga 15% ya Mapato ghafi ya Taasisi za Umma kuwa Mapato ya Serikali kuingia Mfuko Mkuu wa Hazina. SIO FAIDA maana mashirika haya mengi hayana faida. Faida ya TCRA ni nini? Ama EWURA? Ama TANROADS?
Kusema Rais anakabidhiwa gawio la faida ya mashirika ya umma ni ulaghai ambao hauna maana yeyote, kwani Taarifa za Ukaguzi za Mashirika hayo zitaonyesha kuwa hakuna faida (na hivyo hakuna gawio), na hivyo kuumbuka kwa Serikali yenyewe.
Kinachotolewa ni nini? Haya ni maduhuli tu, ama ni kodi maalumu ambayo imewekwa kwa mashirika kwa kiwango cha 15% ya Mapato ghafi. Maduhuli au kodi hii imekuwa ikilipwa miaka yote ya nyuma. Sielewi ni kwanini sasa Rais amewaleta mbele wakuu wa mashirika Eti kutoa gawio! Gharama za kuwaleta hao wakuu wa hizi taasisi hazikupaswa kuingiwa kabisa, kwani kodi hizo hukatwa moja kwa moja kuingia Mfuko Mkuu wa Serikali. Sielewi hizi hadaa ni za Nini?
Ni muhimu pia kueleza kuwa kuna hoja ya Ukaguzi ya CAG kuhusu makato haya kwa baadhi ya taasisi. Kwamba makato haya yanapaswa kuwa ‘Tax deductibles’ – yaani wakati wa kukokotoa kodi ya Mapato ya baadhi ya Mashirika malipo haya yanapaswa kuondolewa kwanza.
Hata hivyo TRA wamekuwa hawafanyi hivi na hivyo kukuta mashirika kama TANAPA, NCAA, TPA nk yanalipa Fedha zaidi ya yanavyopaswa kulipa na kusababisha shughuli zao za msingi kushindwa kutekelezwa.
Watanzania msihadaiwe leo, hatupokei gawio, bali tunapokea maduhuli tu.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Julai 23, 2018.