Mshambuliaji mpya wa Manchester United, Rasmus Hojlund, amefunguka kuwa klabu yake ya sasa ilikuwa ni chaguo la kwanza na si kwingine.
Manchester United ilifanikiwa kumsajili Hojlund kutoka Atalanta katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu baada ya kushinda vita kutoka klabu kadhaa zilizokuwa zikiiwania saini ya straika huyo.
Mshambuliaji huyo kwa mara ya kwanza aliichezea Manchester United ndani ya Premier League dhidi ya Arsenal wakipoteza kwa mabao 3-1. Aliingia uwanjani akitokea benchi.
Hojlund amenukuliwa akisema: “Najua kuna timu nyingi zilikuwa zikinihitaji, lakini Manchester United ndiyo ilikuwa ni chaguo langu la kwanza.
“Sikutaka kwenda kwingine, ni bora ningebaki nilipokuwa kama ningeshindwa kuja Manchester United. Malengo ni kuona naipambania timu yangu kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.”
Hojlund mwenye miaka 20, ametua Man United kwa Pauni 72m, hakufanikiwa kucheza mechi za awali kwa sababu alikuwa majeruhi.