Watu katika kijiji cha nyumbani kwa bibi yake Kamala Harris nchini India, wamekuwa wakisherekea baada ya kutangazwa matokeo kuwa Joe Biden ameshinda katika uchaguzi wa Rais wa Marekani na Kamala Harris kuwa makamu wake.
Kamala mwenye umri wa miaka 55, alizaliwa Oakland, California, na wazazi wahamiaji mama yake akiwa ni Muhindi na baba yake Mjamaica.
Ushindi wake kama mwanamke wa kwanza Makamu wa Rais wa Marekani haswa akiwa mmarekani mweusi mwenye asili ya Asia umepokelewa kwa hisia tofauti za furaha katika maeneo mbalimbali Duniani.
Mwanamke mmoja katika eneo ambalo bibi mzaa mama wa Kamala Harris alizaliwa, aliandika kwa unga wa rangi nje ya nyumba yake: “Hongera Kamala Harris. Fahari ya Kijiji chetu. Vanakkam (salamu) Amerika.”
Maombi yametolewa katika maeneo mbalimbali ya ibada mjini hapo , matangazo ya barabarani yakiwa na picha za Harris.
Harris amekuwa mwanamke wa kwanza Mmarekani mweusi mwenye asili ya Asia kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais katika historia ya Marekani.