Hatimaye bondia wa Australia, Jeff Horn ambaye alikuwa mwalimu shuleni ameishangaza dunia kwa kumpiga bondia Mfilipino mwenye cheo cha Useneta, Manny Pacquiao na kuendeleza rekodi ya kutoshindwa pambano.
Horn (17-0-1) ambaye alikuwa hapewi nafasi na wadau wa masumbwi duniani kwenye pambano hilo lililomalizika dakika chache zilizopita, amemnyang’anya Pacquiao mkanda wa ubingwa wa ngumi wa dunia wa WBO wa uzito wa welterweight baada ya raundi 12 nzito za pambano hilo lililofanyika nchini Australia kwenye uwanja wa mpira na kuhudhuriwa na zaidi ya watazamaji 55,000.
- Picha: Messi alivyofunga ndoa ya kifahari na rafiki yake wa utotoni
- Magazeti ya Tanzania leo Julai 2, 2017
Majaji wa pambano hilo wamempa ushindi Horn dhidi ya Pacquiao kwa point 117-111 & 115-113 (X2), huku pambano hilo likitawaliwa na damu kutoka kwenye majeraha yawapiganaji hao. Ilikuwa ni vita kama ilivyoahidiwa na wote.
Alipoulizwa kama anahitaji pambano la marudiano, Horn ambaye alionekana kucheza ‘rafu’ katika raundi nyingi alijibu, “niko tayari, leteni tena [pambano la marudiano].”
Kwa ushindi huo, Horn ambaye alikuwa anatajwa na wadau kama bondia asiyejulikana, ameingia rasmi kwenye mkondo mkuu wa masumbwi duniani na sasa anaweza kutajwa kuwa tishio kwa mabondia wengi wenye majina Marekani, na huenda akaingia kwenye rekodi ya wanaoweza kupambana na Floyd Mayweather.
Kwa Pacquiao, kupoteza pambano hili ni pigo kwa ndoto yake ya kutaka pambano la marudiaono dhidi ya Mayweather ambaye amerejea akijiandaa na pambano kati yake na bingwa wa UFC, Conor McGregor.