Bondia wa Australia aliyemvua Manny Pacquiao ubingwa wa dunia uzito wa ‘welterweight’, Jeff Horn amesema kuwa bondia huyo anapaswa kupimwa mkojo kubaini kama anatumia dawa zisizoruhusiwa michezoni kabla ya pambano lao la marudiano.
Kambi ya bondia huyo imesema kuwa ina wasiwasi kuwa Pacquiao anaweza kutumia dawa za kuongeza nguvu ili kupata mwanya wa kushinda pambano hilo la marudiano, hivyo imetaka vipimo vifanywe bila kufuata mpangilio maalum (randomly).
Kocha wa Horn, Glenn Rushton amesema kuwa hakuridhishwa na utaratibu uliofanywa wa kupima mkojo wa mabondia hao kabla ya pambano lao la kwanza, ingawa hakuna kati yao ambaye alikutwa na tatizo la kutumia dawa za kuongeza nguvu.
- Mfumo washindwa kuhimili kamali ya pambano la Mayweather Vs McGregor
- Mkongwe Wa Ligi Ya England Kuhamia The Hawthorns
Horn amekaririwa akidai kuwa anajua Pacquiao ameshajua uwezo wake na anafahamu kuwa hataweza kushinda pambano lao la marudiano, hivyo anaweza kufanya ujanja wowote kushinda pambano hilo.
Rushton amesema kuwa ana uhakika Horn atampiga Pacquiao zaidi ya ilivyokuwa kwenye pambano la kwanza na kuondoa misuguano ya utata wa matokeo iliyojitokeza awali.
“Kupima mkojo bila kufuata utaratibu ni kitu nitakachokiibua kwenye makubaliano yetu kwa sababu ambacho sitaki ni wao kuwaza kuwa ‘njia pekee ya kushinda hili pambano ni kama tutatafuta ujanja wa kumzidi’,” Rushton anakaririwa na mtandao wa smh.
“Tunahitaji pambano kubwa, lakini tunataka uwanja wa pambano uwe katika hali nzuri kwa wote,” aliongeza.
Pambano la marudiano kati ya Horn na Pacquiao limethibitishwa na pande zote mbili lakini bado wanaendelea na mjadala wa sehemu ambayo pambano hilo litafanyika na ratiba nzima ya pambano ingawa imewekwa wazi kuwa ni mwaka huu.